SWALI:
Ndugu zangu waislam, Ningependa kujua saa za kula daku ni mwisho saa ngapi
JIBU:
Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.
Daku unaweza kula saa yote hadi inapoingia Alfajiri. Hii ni kutoka na kauli ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala):
((..وَكُلُواْ وَاشْرَبُواْ حَتَّى يَتَبَيَّنَ لَكُمُ الْخَيْطُ الأَبْيَضُ مِنَ الْخَيْطِ الأَسْوَدِ مِنَ الْفَجْرِ ثُمَّ أَتِمُّواْ الصِّيَامَ إِلَى الَّليْلِ...))
((…Na kuleni na kunyweni mpaka ubainike kwenu weupe wa alfajiri katika weusi wa usiku. Kisha timizeni Swawm mpaka usiku…)) [Al-Baqarah: 187]
Hivyo, unaruhusiwa kula daku hadi Alfajiri ndipo unapoanza kufunga. Na hata Muadhini akiadhini nakama una tonge au fundo la maji mdomoni usiliteme, kamilisha kulimeza kisha ndio uanze kufunga. Haya yamethibiti katika Sunnah kama inavyoonyesha Hadiyth ifuatayo:
عن ابن عمر رضي الله عنهما قال: كان لرسول الله صلى الله عليه وسلم مؤذنان: بلال وابن أم مكتوم .فقال رسول الله صلى الله عليه وسلم ((إن بلال يؤذن بليل فكلوا واشربوا حتى يؤذن ابن أم مكتوم)) متق عليه
Kutoka kwa Ibn 'Umar (Radhiya Allaahu 'anhuma) ambaye amesema: "Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa na waadhini wawili; Bilaal na Ibn Ummi Maktuum. Akasema: ((Hakika Bilaal anaadhini usiku (adhana ya mwanzo), basi kuleni na mnywe hadi aadhini Ibn Ummi Maktuum)) [Al-Bukhaariy na Muslim]
Na Allaah Anajua zaidi
SWALI:
Je, Unaruhusiwa kuendelea kula daku wakati Muadhini anaadhini adhaan ya pili? Au hairuhusiwi?
JIBU:
Alhamdulillah.
Inategemea kama Muadhini anaadhini kwa ajili ya Alfajiri (anatoa Adhaan ya kuwa Alfajiri imeshaanza [Adhaan ya pili]), basi lazima usimame kula na kunywa kwa sababu Mtume صلى الله عليه وآله وسلم amesema, ((Msisimamishe daku yenu mnaposikia adhaan ya Bilaal, kwani yeye anaadhini usiku, kwa hiyo kuleni na kunyweni mpaka Ibn Umm Maktuum aadhini)) Na hii ni kutokana na aya (ambayo inaleta maana hiyo)
}}وَكُلُواْ وَاشْرَبُواْ حَتَّى يَتَبَيَّنَ لَكُمُ الْخَيْطُ الأَبْيَضُ مِنَ الْخَيْطِ الأَسْوَدِ مِنَ الْفَجْر{{
{{Na kuleni na kunyweni mpaka ubainike kwenu weupe wa alfajiri katika weusi wa usiku}} Al-Baqarah: 2:187
Vile vile ikijulikana kama Alfajiri imeingia kama mfano mtu akiwa kwenye jangwa basi aache kula na kunywa hata kama hakusikia adhaan (mahali ambapo adhana haisikiki).
Lakini kama Muadhini anaadhini mapema au kama kuna shaka kama adhaan imelingana na Alfajiri au sio, basi unaweza kula na kunywa mpaka utakapokuwa na uhakika kuwa Alfajiri imeshaanza, ikiwa inajulikana hivyo kutokana na ratiba yenye kutegemewa au kutokana na Muadhini mwenye kuaminika anayejulikana kuwa anaadhini wakati wa Alfajiri. Kwa hali hii (ikiwa adhaan imeadhiniwa mapema sana) unaweza kula wakati adhaan inaadhiniwa, ule au unywe kilichokuweko mkononi mwako kwa sababu hakuna hakika kama adhaan inaadhiniwa kwa wakati wake ulio sahihi, bali huenda kulikuwa tu ni kwa makisio na si kwa uhakika.
Majmu'u Fataawa ash-Shaykh Ibn Baaz, mjalada 15, ukurasa 282.
SWALI:
Kuhusu kula daku, hapo naomba ufafanuzi hasa maana huku sisi hatuswali Alfajir twaswali Assubhi, sasa tukiwaruhusu watu kula mpaka wakati wa adhana ya mwisho mi nahisi tutakuwa tushawalisha watu mchana. Wajua hawa watu wanaoandaa nyakat za swala wao wenyewe wanasema tufanye makadirio ya nyakati swala. Naomba unifafanue pia hapo.
JIBU:
Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘Alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.
Shukrani zetu kwa swali lako la nne. Kuhusu ufafanuzi wa swali la:
Ndugu kwa wakati huu wetu wa sasa tunafaa tusiwe na utata wowote kwani waliotutangulia wlifanya bidii kwa kufanya utafiti hadi wakatuwekea jedwali ya machomozo ya jua na machweo yake.
Ni vizuri kuwa na jedwali ya mwaka mzima na kutazama wakati wa kuingia Alfajiri ya kweli ambao ndio wakati wa uhakika wa adhana ya pili. Katika kipindi cha hasa Ramadhaan maratibu wa Msikiti wenu mzungumze na kamati au Imaam aelezwe mwadhini wakati wenyewe na hapo hakutakuwa na utata wowote. Labda tukitoa mfano itaeleweka zaidi nayo tukichukua wakati wa adhana ya pili na machweo kwa mji wa Mombasa ambao nyakati zake zitakaribiana na Dar es Salaam . Kwa tarehe 10 Oktoba 2007 adhana ya pili ilikuwa saa kumi na dakika 49 ilhali machweo ni kumi na mbili (12) na dakika 13. Hatudhani kuwa jedwali kama hizo hazipo Dar na hata kama hazipo kwa uzoefu wa Waislamu nyakati za kula na kusitisha kula hazitakuwa ni zenye kuwashinda wao au kutojua.
Allaah (Subhaanahu wa Ta‘ala) Anasema kuhusu nyakati hizo:
“Na kuleni na kunyweni mpaka ubainike kwenu weupe wa alfajiri katika weusi wa usiku. Kisha timizeni Swawm mpaka usiku” (2: 187)
Huu ni muongozo tosha kwetu sisi na kukosea kwa baadhi ya watu katika kufuata hayo haifai kutufanya sisi kutoweza kutotekeleza ‘Ibaadah zetu. Hapa Allaah (Subhaanahu wa Ta‘ala) Ametupatia nyakati za kuweza kufunga na mwenye kuelewa huwa hana tatizo. Mwisho wa kula ni kubainika kwa weupe wa Alfajiri, na huo ni weupe wa pili ambapo wakati wa Swalah hiyo huwa umeingia. Unapopatikana weupe huo basi inafaa usitishe kula lakini ikiwa unakula ukiwa na hakika kuwa bado Alfajiri kuingia kisha ukashtuka kuwa umekosea hilo halitaathiri Swawm yako ya siku hiyo. Mwisho wa kufunga ni kuingia usiku kwa kuchwa kwa jua na haifai kuongeza dakika 5 au 10 kwa kisingizio cha kuhakikisha kuwa kweli jua limekuchwa. Jua likizama tu mfungaji anafaa afungue.
Lakini kama tulivyosema hapo juu ni kuwa tatizo hili linafaa lisiwepo kwa ajili ya juhudi zilizofanywa kuhusu suala hilo kwa miaka mingi.
Na Allaah Anajua zaidi
SOURCE; ALHIDAAYAH.COM
No comments