![[âIMG]](https://blogger.googleusercontent.com/img/b/R29vZ2xl/AVvXsEhjBSVxgPQCBXlsZmQqieVJ8fL3BsmWQca4Kn2til4P881u6Xs-6lSMlsFVvESws_uW5t2MO5NsMIU6tCMtWEB2ioL_lzXOG8hQrPPeKXpT73-rKIP8Te2GUSphXncvow8JaUFQqER0O9c/s640/0a.jpg)
SIMULIZI : USIKU WA JAN .20,2005 SEHEMU YA PILI
MTUNZI; INNOCENT A. NDAYANSEE
“Joka hilo!” alisema. “Nina wiki kama tatu hivi tangu liniume. Nilikuwa nimekaa hapo nyumbani, nje nikipunga hewa. Likatokea huko lilikotoka, kasi ile mbaya, liliponifikia tu likaning’ata na kuteleza msh’kaji wangu. Jeusi na refu kishenzi! Nilipiga kelele mshkaji wangu, akaja faza na kijiwe f’lani hivi sijui kakitoa wapi… akaniwekea mguuni, nasikia huwa kinafyonza sumu.
“Halafu wakanipeleka Agakhan Hospital. Ningekufa! Yaani ni kama niliponea chupuchupu! Wiki nzima sikuweza kutembea. Sasa nimepona lakini cheki nimekuwa kama nyoka au kenge kudadek! Magamba haya nd’o yanatoka…sijui nd’o ngozi iliyoharibiwa na sumu?!”
Nilimwelewa lakini sikumjibu kitu. Mawazo yangu yalikuwa juu ya zahama iliyonikuta. Nikamkumbuka mke wangu. Nikawaza, je, atawaza kuwa niko wapi? Anaweza kuwa na mawazo dhaifu akafikiria kuwa nimekwenda kwa mwanamke wa pembeni? Nimpigie simu?
Swali hili la mwisho nikaona ndilo linapaswa kufanyiwa kazi. Hata hivyo, usalama kwanza! Ndivyo nilivyoamini. Nikatulia huku nikiyasikilizia maumivu ya jeraha na zile chale ambazo nazo ziliongeza maumivu huku nikizidi kutishika kila nilipoutazama mguu huu na kushuhudia damu hiyo yenye mabonge-bonge mazito ikizidi kutoka kwenye yale maeneo yenye chanjo za wembe.
Gari likaenda hadi eneo la Mkwajuni ambako tuliingia katika zahanati moja ya MICO. Daktari akatupokea kwa moyo mkunjufu na kuniangalia kwa macho ya huruma. Baada ya kupata maelezo akasema, “Ni tatizo kubwa kwa upande wetu hapa kwenye zahanati. Sisi hatuna uwezo wa kukuhudumia lakini kwa kupunguza tatizo ili sumu isiende kudhuru figo, nitakuchoma sindano moja ya kinga halafu itabidi uende Mwananyamala.”
Wale wasamaria walionileta waliposikia hivyo wakamshukuru daktari na kuniambia kuwa wao wanarudi nyumbani kwa kuwa hata gari lao halina mafuta ya kuweza kunipeleka huko Mwananyamala.
Nikajua kazi ninayo. Hata hivyo, nikawashukuru kwa msaada huo wa kunifikisha hapo. Nikajali kwanza kupata huduma hiyo ya sindano. Na nilipokwishachomwa, nikatoka nje na fimbo yangu dhaifu huku bado damu ikizidi kunitoka kwa wingi na baadhi ya watu wakawa wakiniangalia kwa mshangao bila ya msaada.
Nikaanza kujikokota nikielekea kituo cha daladala huku nikiwaza je, kuna daladala itakayonikubali kwa hali ile niliyokuwa nayo? Guu limeshavimba na limetapakaa damu nyeusi ti! Nikajisikia kukata tena tamaa!
Nikajikokota tu bila ya matumaini hatua kama kumi hivi, jamaa mmoja akanisimamisha na kuniuliza, “Vipi aisee?”
Nikamtazama na kugundua kuwa ni fundi makenika ambaye tulikuwa tukikutana mara kwa mara jirani na Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Usharika wa Azania katikati ya jiji akitengeneza magari katika kijigereji bubu kilichokuwa katika eneo hilo. Jamaa huyo ambaye siwezi kulisahau jina lake, Lyimo, alikuwa msaada mkubwa kwangu kwa siku hiyo.
Japo tulifahamiana, lakini hatukuwa na ukaribu, ni kule kujuana-juana tu kimjini-mjini kama ilivyo kwa wakazi wengi wa Jiji la Dar. Lakini usiku huu wa saa tatu kasoro jamaa huyu alisitisha kuendelea na safari pale tu nilipomdokeza mkasa ulionikuta.
Hatua chache kutoka pale tulipkuwa kulikuwa na teksi mbili zimeegeshwa. Haraka akamwita teksi dereva mmoja na kumwambia, “Danny, mpeleke mshkaji wangu Mwananyamala hospital haraka.”
Dereva yule aliniangalia kwa mshangao na kuniuliza, “Umekumbwa na mkasa gani?”
“Huu siyo muda wa maswali!” Lyimo aliingilia kati. “Mpeleke halafu ukirudi uje kuchukua pesa yako.”
Dereva alinifungulia mlango wa kushoto, mbele huku akiniambia, “Ingia msh’kaji.”
Kisha Lyimo akaniuliza, “Nyumbani wana taarifa?”
Ni hapo nilipojiwa na kumbukumbu kuhusu umuhimu wa kufikisha taarifa nyumbani. Nikamjibu kuwa hakuna taarifa na nikampa namba mbili za simu, moja ya rafiki yangu na nyingine ya mke wangu.
“Simu yangu haina salio na inaweza kuzima muda wowote,” nilimwambia. “Tafadhali, ukiweza nisaidie kuwapigia kuwapa taarifa.”
“Usijali nitahakikisha taarifa inafika. Nikishindwa basi nitapita hata pale kanisani na kuwataarifu.”
Teksi iliondoka na kwa kweli yule dereva alikuwa na moyo wa kibinadamu zaidi kwani tulipofika Hospitali ya Mwananyamala hakuniachia getini. Alinishika mkono na kunipeleka hadi kwa daktari huku wagonjwa wengine wakituruhusu kuwapita kwa kuwa hali yangu iliwatisha na kuonekana kuwa napaswa kupewa kipaumbele katika huduma.
Baada ya kutoa maelezo kwa dakatri, nikakalishwa kwenye kiti maalum na dereva huyohuyo wa teksi, akanisaidia kwa kukisukuma kiti hicho hadi wodi namba 5 ambako nilikabidhiwa kitanda. Usiku huo wa Alhamisi ukanikuta hapo hospitali na ukaisha nikiwa hapo hospitali.
Siku iliyofuata ilikuwa ni Sikukuu ya Maulid. Siku ya mapumziko. Mimi nilikuwa wodini. Ndugu, jamaa na rafiki walifika hospitali kuniona. Wanakwaya wengi pia walifika kuniona. Lakini hadi kufika jioni sikuwa nimepata huduma yoyote kubwa kuhusu jeraha hilo zaidi ya kupewa tembe za kutuliza maumivu! Mguu ulizidi kuwa mweusi hususan eneo la kiganjani. Na uvimbe ulizidi!
Kila nilipojaribu kuhoji kwa nesi kuhusu kuhudumiwa nilipata majibu yasiyoelewaka. Mara, “Dokta atapita…” mara “vuta subira madokta wako kwenye kikao…” mara hili mara lile ilimradi yalikuwa ni majibu yasiyokuwa na msaada wowote kwangu.
Hatimaye usiku ukaingia bila ya kupata huduma yoyote! Ilipofika saa 4 nesi mmoja akaniletea vidonge vya vallium ili nipate usingizi. Nikanywa na vikanisaidia kwa kiasi fulani.
Asubuhi ya siku ya Jumamosi mambo yakawa vilevile. Hadi saa 4 bado sikuwa nimemwona daktari yeyote aliyefika kunihudumia. Kungekuwa na mgomo rasmi uliotangazwa na madaktari labda ningeelewa lakini hakukuwa na mgomo wa wazi labda wa siri.
Hatimaye saa 7 mchana ikatinga, bado sijaona mtu. Nilipoletewa chakula kutoka nyumbani nikala kama kawaida kwani jeraha lile halikunifanya nishindwe kula. Lakini nilishangazwa na huduma za hospitalini hapo. IIipotimu saa sita hivi nikamwona mwanamume mmoja amevaa joho jeupe la kidaktari akipita kitanda kimoja hadi kingine. Hatimaye akafika kwangu na kukiangalia cheti kwa muda kisha akaandika-andika maandishi aliyoyajua mwenyewe kisha akawa ananiangalia mguu hatimaye akaondoka. Sikumwona tena kwa siku hiyo na wala sikumwona muuguzi yeyote mwingine.
Usiku saa 4 nikapewa tena vallium ili nisinzie!
Nikasinzia.
Asubuhi ya siku ya Jumapili nikawa nimekwishakata tamaa ya kuhudumiwa katika hospitali hiyo kubwa zaidi ya serikali wilayani Kinondoni.
Wakati kaka yangu Barack (sasa ni marehemu) alipokuja akifuatana na rafiki yangu mkubwa, askari wa JWTZ, Mathew Mapunda SAA 7 mchana, tayari nilikuwa nimekuwa na uamuzi wa kuondoka hospitalini hapo. Na wao walipofika walikuwa na wazo kama langu. Hata hivyo, kabla ya kuchukua uamuzi, tulimuuliza nesi mmoja aliyekuwa akirandaranda humo wodini, nesi ambaye kwa kiasi fulani nilikuwa nimekwishazoeana naye.
“Ni kwa nini sijahudumiwa mpaka leo?”
Nesi yule alitabasamu kidogo kisha akaniambia kwa sauti ya chini, “Kaka si kwamba madaktari hawapo …wapo sana..wamejaa tele ka’ pishi ya mchele. Wanajichimbia kule theatre (chumba cha upasuaji) wakingoja dili. Kama una pesa leta nikamwone daktari aje akuhudumie. Vinginevyo kaka’angu…mmmh” akaiacha sentensi hiyo ikielea.
Nilimwelewa.
Kaka yangu na rafiki yangu walikuwa na pesa lakini kwa hasira yule rafiki yangu alisema, “Hapa hapafai! Hakuna kutoa pesa wala nini…tuondoke zetu!” akamgeukia yule nesi na kumwambia kwa ukali, “Tunaondoka na mgeni wetu!”
“Hatukatai lakini subirini basi tufanye utaratibu wa ‘kumdischaji’.”
“Nini?! Hatuna muda mchafu!” kaka yangu alifoka huku akipunga mkono hewani. “Hatusubiri chochote! Tunaondoka naye!”
Mathew na kaka yangu wakatoka, wakielekea nje ya geti. Wakati huo wanakwaya takriban kumi na watano nao walikuwa nje ya wodi wakiwa wamekuja kunijulia hali na kujua hatima ya sakata lililonikabili.
Dakika chache baadaye kaka yangu na Mathew wakarejea wakiwa ndani ya gari pick-up, nikapanda na wanakwaya wengine wakapanda tukasepa!
Moja kwa moja hadi Kinondoni Mtaa wa Sekenke ambako kulikuwa na zahanati iliyokuwa ikisifiwa kipindi hicho; Nyamongo. Ile kufika tu nikapewa tembe moja ndogo kisha nikachomwa sindano moja. Nikapewa kitanda ndani ya chumba nikiwa peke yangu!
Nikalazwa kwa mara ya pili!
Nikatundikiwa dripu tatu mfululizo! Jumatatu asubuhi, Januari 24 nilikuwa na nafuu kubwa. Japo maumivu ya mguu bado yalikuwapo lakini hayakuwa ya kutisha! Na ilipofika jioni niliruhusiwa kuondoka.
SIKU MBILI BAADAYE
Wakati nikiwa nyumbani nikiuguza jeraha walikuja watu kadhaa kunijulia hali. Baadhi yao ndio waliozungumza kuhusu tukio la nyoka yule na imani za kishirikina. Kuna waliodai kuwa joka lile lilikuwa likifugwa na mama mmoja wa Kiarabu aliyekuwa akiishi jirani sana nyumba ya Shule ya Msingi Hananasif, na kwamba mama huyo alikuwa amechoka kuendelea kumfuga hivyo akamwachia.
Ikadaiwa kuwa nyoka huyo amekwishawauma watu wanne, mimi nikiwa mmojawao kwa kipindi cha wiki mbili!
Na ikaendelea kudaiwa kuwa mara kwa mara kila ifikapo usiku pale kwenye makutano ya Barabara za Wakulima na Ngano, jirani kile kijibaa, husikika kelele za kicheko cha mwanamke asiyeonekana!
Siku ya tatu gazeti maarufu kwa siku zile, ALASIRI lililokuwa likichapwa na kampuni ya The Guardian Ltd, likachapa kwa kirefu habari yeny kichwa cha: JOKA LA MAAJABU LAITIKISA HANANASIF. Habari hiyo ikawafanya wakazi wengi wa eneo hili wagwaye kupita Barabara ya Ngano iwe asubuhi mchana hata jioni au usiku.
Ni wengi walioogopa siyo wote. Baadhi walipita lakini wakiwa na hadhari kubwa na kikafika kipindi kila mtu alikuwa akipita mtaani hapo macho yake yanakuwa juu ya miti akihofia kuwa huenda joka hilo liko mtini na linaweza kumshukia mtu yeyote.
Siku mbili baada ya gazeti hilo kutoa habari hiyo, dada mmoja (sasa ni marehemu) aling’atwa na nyoka njiapanda ya barabara hizo za Wakulima na Ngano zikiwa ni kama hatua hamsini tu kutoka pale nilipong’atwa mimi.
Huyo hakuwa peke yake, alikuwa na mdogo wake ambaye alihadithia simulizi isiyotofautiana na madhila yaliyonikuta mimi ile Januari 20. Kwamba, muda mfupi baada ya dada yake kuumwa na nyoka, kicheko kikali kikasikika kutoka kwenye mkusanyiko wa miti uliounda chaka zito kwenye makutano hayo.
Kisha kukazuka upepo mkali kwa muda mfupi na kutoweka. Lakini tofauti ndogo ni kuwa siku hiyo hakukuwa na mtu aliyezuka mbio na kuwapita pale kama ile siku yangu na yule mwanamke.
Hata hivyo, dada yule ambaye alikuwa akiishi hukohuko Hananasif alikata roho muda mfupi baada ya kufikishwa hospitali huku mwili wote ukiwa umebadilika rangi na kuwa mweusi ti!
Wiki moja baada ya dada huyo kufariki nikapata taarifa kuwa hata yule kijana wa Kiarabu ambaye alinipa msaada wa kunipeleka Hospitali ya MICO pale Mkwajuni kwa huduma ya awali, akiwa na mguu wake uliobabuka ngozi kutokana na sumu ya nyoka naye amefariki! Sababu, mguu wake ulivimba tena na kubadilika tena rangi, ukawa mweusi zaidi kisha mwili wote ukavimba na alikata roho ndani ya saa ishirini na nne tu!
Nikahofia kuwa labda na mimi niko kwenye mkumbo huohuo kwa kile kilichoaminika kwa wakazi wa hapo kuwa yule hakuwa nyoka wa kawaida, ni joka la miujiza. Ni jini!
Mtaa huo ukawa ukiogopwa na wakubwa kwa wadogo. Nilithibitisha kuwa mtaa huo ulikuwa ukiogopwa na watu kwa kipindi hicho siku nilipopewa lifti ya gari nikielekea maeneo ya Posta Mpya na kutomwona mtu hata mmoja akitembea barabarani hapo hadi Mwembejini!
Hata akinamama waliokuwa wakipeleka biashara mjini maarufu kwa ‘mamantilie iliwalazimu kukusanyana hadi kufikia kumi au zaidi kisha wanasindikizwa na wanaume wawili au watatu wakiamini kuwa ndiyo salama yao!
Mtaa wa Ngano ukageuka kuitwa kimasihara kwa jina LA ‘Mtaa wa Nyoka!’
Guu langu liliendelea kuwa jeusi japo halikubabuka. Mwezi ukaisha nikiwa siwezi kuvaa kiatu. Mwezi wa pili ukakatika! Lakini nafuu ilizidi kupatikana. Hatimaye siku ya Jumapili ya Pasaka mwezi Aprili, nikafumba macho na kuvaa viatu huku nikijisemea ‘liwalo na liwe’ kama ni kukatwa mguu basi na nikatwe.
Nilifikia hatua ya kuchukua uamuzi huo kwa kuwa kuna daktari mmoja alinihadharisha kuwa nikivaa kiatu wakati bado sumu haijateketea mguuni basi mguu utaoza!
Nilishachoka kupita mitaani na sandozi!
Siku hiyo ya Pasaka nikavaa viatu na kwenda kanisani. Ukawa mwanzo wa kupona. Badala ya maumivu kuongezeka, yakawa yanapungua kila kukicha. Taratibu rangi ya ngozi ikaanza kurudi. Hadi leo niko vizuri na mtaani hapo kuko kawaida. Mtaa unapendeza maradufu!
Hakuna wa kuumwa nyoka wala tandu! Tofauti ni kuwa ile miti iliyopandwa kando ya barabara imekuwa mikubwa zaidi na imestawi zaidi, kiasi cha kutoa taswira ya kuvutia machoni mwa yeyote apendaye mazingira ya aina hiyo. Kijani kitupu! Mchana kuna kivuli kizito!
Sasa ukipita usiku barabarani hapo giza lake ni zaidi ya giza. Kama una moyo mwepesi, utageuza njia urudi ulikotoka!
*****MWISHO.*****
MWANDISHI:
MHUSIKA: INNOCENT A. NDAYANSE
No comments