KISA CHA NABII MUSA(A.S) NA HIDHIRI
sehemu ya 03
....Wazee wao. Mbinu kama hizi mara nyingi zimetumika kuwahadaa watu wenye upeo mdogo wa kufikiri, Hata wapinzani wa Mtume Muhammad, Makka walitumia mbinu za aina hiyo.
Lakini kinyume na matarajio ya Firauni, kwa hekima, Musa alijibu kuwa habari za watu hao wa zamani anazijua Mwenyezi Mungu ambaye ana rekodi ya kila jambo katika kitabu chake na hana udhaifu wa kupoteza kumbukumbu. (20:52) Kama Musa angejibu kuwa watu hao wa zamani walikuwa wapotevu na hivyo watakuwa kuni za Jahanamu lingemsaidia Firauni kufikia lile lengo lake alilokuwa nalo kichwani wakati alipoulizwa swali. Baada ya jibu la Musa kumvurugia shabaha yake, Firauni sasa akamtaka Musa atoe hoja za kuthibitisha ukweli wa madai yake (7:106). Ndipo Musa alipoonesha miujiza, Kwanza alitupa fimbo yake ambayo iligeuka nyoka (7:107) na kisha akatoa mkono wake ambao ulikuwa unang'ara (7:108).
Kuona miujiza hiyo, Firauni akachanganyikiwa na kuuliza kwa hamaki, "kumbe wewe Musa umekuja kututoa nchini mwetu kwa nguvu za uchawi wako (20:57). Hapa Firauni alitumia mbinu nyingine ya kujinusuru na hatari ya Musa. Badala ya kusema, umetujia na miujiza, yeye akasema umetujia na uchawi. Lengo lake lilelile la kuvuruga mazingatio ya watu waliokuwa wakitazama kwamba waione ile miujiza kama uchawi tu ambao hata watu wengine wa kawaida wengeweza kuufanya. Kwa mbinu hiyo, angevunjilia mbali hoja ya ile ya miujiza ambayo ingethibitisha utume wa Musa na hivyo kuwafanya watu wamkubali Mungu aliyemtuma mtume huyo jambo ambalo lingeshusha hadhi ya 'uungu' ya Firauni na kumpotezea nguvu zake za kisiasa na hatimaye madaraka yake.
Ifahamike kuwa, Firauni alikwishabaini kuwa Musa alikuwa na dalili za Utume, kwa maana hiyo, alikwishadhihirikiwa na ukweli wa yale yote aliyokuwa akiyasema Musa. Lakini alikuwa anakwepa kukiri kwa hofu ya kupoteza ufalme wake.
Maelezo ya historia ya Musa katika Qur'an inaonesha kuwa Musa alipelekwa kwa wakuu wa Misri yaani Firauni, Amana na Karuni akiwa na muelekeo wa wazi wa kupiku mamlaka yao yaliyosimamia juu ya msingi wa dhana ya uungu bandia.
Kwanza, kule kujitokeza kwa Musa mbele yao bila hofu licha ya kukabiliwa na jinai ya kuua mtu wa Taifa la Firauni. Musa alilazimika kukimbilia nchi nyingine kujificha baada ya Firauni kutoa amri akamatwe. Sasa iweje mtu huyo aibuke na kwenda moja kwa moja Ikulu si kwa minajili ya kuomba msamaha bali kwa lengo la kumtaka Rais na Mawaziri wake wamtambue kuwa yeye ni Mtume wa Mungu Muumba wa ulimwengu na kwamba wao watawala waache sheria na kanuni au sera zao na badala yake wafanye vile atakavyo Mungu.
Ujasiri huo tu ulitosha kuwa ishara ya utume wa Musa. Isingelikuwa rahisi kwa mtu wa kawaida tena basi mwenye hatia ya mauaji kuwakabili watawala namna hiyo. Isitoshe taifa la Musa lilikuwa dhaifu au tuseme nyonge chini ya utumwa hivyo hatakama Musa angekamatwa na kuhukumiwa kifo, lisingeweza kumtetea kwa namna yoyote ile. Na huenda baadhi yao wangemlaumu kwa jaribio hilo hatari!
Kwa hali hiyo, hata kabla ya kuonesha miujiza, Firauni na watu wake walikwishagundua kuwa Musa alikuwa na nguvu fulani kubwa nyuma yake iliyomfanya ajiamini kiasi hicho. Pili, kila muujiza alioonesha Musa ulitofuatiana kabisa na uchawi, Miujiza yote ilidhihirisha nguvu isiyo ya kawaida kwa sababu uchawi hauwezi kugeuza fimbo kuwa nyoka halisi. Ndio maana Firauni na washirika wake wakasema kuwa Musa ni "mchawi" mkubwa (40:24), (7:109). Jina "mchawi mkubwa" kama ilivyokwishaeleza lilificha ukweli kwa sababu za kisiasa. Na tatu, ule uzungumzaji wa Musa uliojaa hekima na hoja zinazoingia akilini nao pia ulidhirihisha ukweli wa maneno ya Musa kuwa yeye ni Mtume. Firauni alikuwa anamjua Musa vizuri sana kwa sababu aliishi nyumbani kwake. Kwa hiyo aliweza kugundua kuwa Musa hakuwa na uwezo wa kuzungumza hivyo kabla ya hapo.
Baada ya Musa kuitia msukosuko serikali ya Firauni, mtawala huyo akataka ushauri kwa washirika wake (26:35). Wakamshauri kuwa akabiliane na Mussa kwa nguvu za uchawi. Hivyo, wakamtaka atume watu wapigao mbiu ya mgambo wakusanye wachawi wote wakubwa yaani 'magwiji' ili kumkabili Musa (26:36-37). Ikumbukwe kuwa kulikuwa na mamia ya wachawi katika nchi hiyo ambao mara nyingi walikuwa wakifanya mazingaombwe kwa lengo la kujipatia zawadi na tuzo. Kwa maneno mengine uchawi, kwa watu hao ulikuwa kama ajira. Ndio maana walipoitwa kwa Firauni wakauliza kuwa wangepata ujira gani kama wangemshinda Musa. (7:113).
Kama ilivyodokezwa awali kuwa, Firauni alikwishaiona hatari ya Musa kisiasa kwamba miujiza ya Musa ingewateka sio tu watu wake wa karibu bali hata wananchi wa kawaida pia. Ndio sababu akakwepa kuita miujiza na badala yake akaiita uchawi na akamwita Musa mchawi stadi (26:34)
ITAENDELEA
INN SHAA ALLAH
ITAENDELEA
INN SHAA ALLAH
No comments