SIMULIZI: USIKU WA JAN. 20, 2005... SEHEMU YA KWANZA

Share:
[​IMG]

SIMULIZI: USIKU WA JAN. 20, 2005 SEHEMU YA KWANZA

MTUNZI : INNOCENT A. NDAYANSE


ILITOKEA kupenda kupiga gitaa tangu nikiwa na umri wa miaka 14. Lakini nilipenda kupiga baada ya kaka yangu ambaye katika familia yetu alitokea kuwa naye karibu takriban kwa kila jambo. Aliitwa Barack Ambrosse Ndayanse.
Barack alikuwa mpenzi zaidi wa gitaa na alikuwa akipiga na rafikiye kipenzi Ramadhani Zahoro, wakitoroka darasani na kwenda kujificha kwenye shamba la mihogo na kuanza kupiga gitaa lililotengenezwa kwa zana hafifu za galoni la lita tano za maji.

Kwa kuwa mara kwa mara nilikuwa nashinda naye, nilishawishika na mimi kujifunza kutekenya nyuzi za gitaa hilo la kienyeji.
Mieze kadhaa baadaye tukajikuta kwenye kwaya ya Kanisa la Anglikana Mwanga mjini Kigoma na wakati huo walikuja wanamuziki wawili kutoka katika kwaya iliyokuwa ikitikisa ukanda wa Afrika Mashariki, Mwanza Town Choir.
Wanamuziki hao walikuwa wamekuja mjini Kigoma kwa ajira za Upanuzi wa Bandari na hivyo wakaamua kuwa wanakuja kanisani hapo kupiga magitaa.
Ni hapo ndipo mimi na Barack tulipogundua kuwa viwango vyetu vilikuwa duni sana na kuanza kujifunza kwa hao vijana waliotoka Mwanza.
Tuliendelea na fani hiyo na mimi nikajikuta nikikomaa zaidi katika gitaa la solo kiasi cha kujikuta nikianza kupiga katika bendi moja iliyokuwa mjini hapo ya Super Kibisa Orchestra tukiwa na Ramadhani Zahoro ‘Bangwe’ ambaye kwa sasa ni mpigaji gitaa tegemeo wa Msondo Ngoma Music Band.
Hata hivyo, baadaye Ramadhani aliondoka Kigoma na kulivaa jiji la Dar es Salaam, mimi na Barack na wanamuziki wengine tukabaki tukiliendeleza ‘sebene’ kwenye bendi hiyo na wakati huohuo pia tukiupiga muziki kwenye kwaya.
Hiyo ni ile miaka ya 1980-1989.

Kuanzia mwaka 1990, kasi ya kupiga muziki ikanipungukia na hiyo ni kwa sababu nilibaini kuwa sikuwa napenda sana fani hiyo bali tu ni kwa ajili ya kuhimizwa na ndugu yangu. Sasa nikahamia jijini Dar es Salaam na nikawa napiga gitaa mara chache pale nilipoliona.
Siku zikaenda hatimaye nikajiunga na Kwaya ya KKKT Hananasif Kinondoni, kwa maombi ya mwalimu mmoja aliyewahi kuniona nikipiga gitaa mahali fulani. Hapa Hananasif nimekaa sana na kwa kuwa ndipo yalipokuwa masikani yangu nikajikuta nikirudi kwenye fani kwa kasi ya ajabu.
Mapenzi yangu kwa mpiga solo mahiri wa enzi za miaka ya 90, Alain Makaba wa Wenge BCBG yakairudisha ile ari yangu ya kupiga gitaa na hasa kwa kipindi kile Wenge walipoibua albamu ya Pentagone mwaka 1994.
Sasa nikarudi kwenye gitaa kwa nguvu kubwa. Kila wimbo uliopigwa na Alain Makaba nikawa nauiga na kwa kiasi kikubwa. Kiwango kikapanda. Mwishoni mwa miaka ya 1990, African Stars ‘Twanga Pepeta’ wakazaliwa. Nakumbuka bendi hiyo ilikuwa inapiga muziki wake kwenye viwanja wa Leaders Club bureee! Kila Jumapili mchana!
Watu tukawa tunajimwaga hapo kila wikiendi na hasa kwa kuzingatia kwangu mimi pale palikuwa ni jirani sana na nyumbani.
Mpangilio mzuri wa muziki wa Twanga sanjari na upigaji wa Adolf Mbinga katika gitaa la solo vilinivuta sana na hivyo sasa nikawa nikibuni vyangu, nachanganya na vionjo vya ama gwiji Alain Makaba au mzalendo Adolf Mbinga hasa na wimbo wake wa Kisa Cha Mpemba.
Nikaendelea kuwa bora katika fani hiyo huku pia nikifanya kazi ya ajira katika Kampuni ya Uchapishaji ya Heko.

JANUARI 20

Hii ilikuwa ni siku, kama siku nyingine ambazo niliamka na kwenda kwenye shughuli zangu za kila siku. Ilipofika jioni, kitu kama saa 11 hivi nikawa nimesharudi Kinondoni na moja kwa moja nikaelekea kanisani kwa ajili ya mazoezi ya kwaya. Mazoezi yalimalizika saa 1 usiku. Kijigiza kilikuwa kimekwishaitawala anga.
Baada ya mazoezi nilitoka na rafiki yangu, Zawadiel Kimambo aliyekuwa akiishi Kinondoni Shamba. Nilikuwa nikimsindikiza na tulikuwa na mazoea ya kuzungumza kuhusu hili na lile hususan kuhusu kwaya kila tumalizapo mazoezi.
Siku hiyo, mara tulipomaliza mazoezi nilichoropoka hadi nyumbani ambako hakukuwa mbali. Nikavua viatu na kuvaa kandambili kwa kuwa siku hiyo sikuwa natarajia kwenda mbali. Nikarudi eneo la kanisa ambako nilimkuta Kimambo akiwa nje ya uzio akizungumza na wanakwaya wengine huku akinisubiri.
Mara tu nilipofika Zawadiel alisitisha maongezi na kuniambia, “Inno twen’zetu.”
Tukaondoka taratibu. Tukapita jirani na shule ya Msingi Hananasif katika eneo lilikokuwa na miti mingi iliyoongeza nguvu ya giza kwa kuwa hakukuwa na nyumba zilizokuwa kando ya barabara.
Tukawa tunashika Mtaa wa Ngano, mtaa uliokuwa umepandwa miti mingi iliyounda kivuli kizito mchana na kutengeneza giza la kuogofya usiku.
Mazingira yale tulikwishayazoea hivyo hatukuwa na wasiwasi wowote. Tukawa tukitembea taratibu huku tukizungumza.
Hatimaye tuliuacha Mtaa wa Ngano tukashika Mtaa wa Wakulima. Mbele kidogo tukawa tunapita katikati ya makaburi. Tulipofika mwisho wa eneo la makaburi, tukawa kando ya Barabara ya Kinondoni, eneo lililojulikana na linalojulikana mpaka sasa kwa jina la MWEMBEJINI.

Hapo tulikuta mchanganyiko wa watu. Walikuwepo waliokuwa kituoni wakisubiri daladala na wengine kwa harakaharaka unaweza kuwaita ‘vibaka’ au ‘mateja kwani walikuwa ni vijana wanne wakizunguka-zunguka tu kituoni hapo huku wakizungumza kwa sauti zenye mikwaruzo inayokera, sigara na bangi zikivutwa bila ya wasiwasi.
Mimi na Zawadiel hatukuwajali kama ambavyo nao hawakutujali. Mara kwa mara watu wa aina ile huwa eneo lile wakivizia daladala ili waingie na kubanana na abiria na matokeo yake abiria ‘hulizwa.’ Au huvizia abiria atakayeteremka na kuzubaa-zubaa na wao huwa wepesi kwa kumpora chochote chenye manufaa kwao.
Tulivuka barabara na kuendelea na safari, nikiendelea kumsindikiza rafiki yangu kipenzi, Zawadiel.
“Tuingie pale kwenye kantini tunywe maziwa moto,” Zawadiel aliniambia mara tulipokuwa upande wa pili wa barabara.
Sikuwa na sababu ya kukataa. Nikamjibu, “Poa tu.”
Tukaingia. Akaagiza maziwa moto na keki mbili. Tukanywa taratibu huku tukiendelea kuzungumzia mambo ya muziki wa gitaa, fani iliyokuwa inayateka maongezi yetu kila tunapokuwa pamoja.
Nusu saa baadaye, kama saa 2 hivi, tuliagana, yeye akaendelea kwenda kwake ambako kwa hapo hakuwa mbali sana na mimi nikaanza safari ya kurejea nyumbani Hananasif. Kumbuka nilikuwa nimetoka nyumbani na kandambili tu miguuni na sikutarajia kuwa ningetembea mpaka huko Kinondoni Shamba.

Hata hivyo, nilijifariji kuwa kwa giza lililokuwapo isingekuwa rahisi kila mtu kubaini kuwa nimevaa nini miguuni. Sikujali. Nikaanza kuvuta hatua, nikavuka barabara huku nikiwa nimekifungua kijiredio changu kidogoooo aina ya Panasonic nikisikiliza muziki.
Wakati niko eneo la katikati ya makaburi, nikimulikwa na mwangaza mkali kutoka kwenye taa kubwa zilizolizingira jengo moja lenye ofisi nyeti sana serikalini, mara nikakutana mwanamama mmoja mnene kiasi akiwa amejitanda kanga kutoka kichwani.
Dada huyo akanichangamkia haraka, “Kaka, mambo?”
“Poa tu,” nilimjibu na kumtazama kidogo kisha nikaendelea na safari yangu. Hakuniachia. “Anko samahani kidogo,” aliniambia huku akiwa amesimama na kunigeukia.

Nikaiheshimu kauli yake. Nikasimama na kumsikiliza.
Akanisogelea. Tukawa jirani sana. Tukatazamana. Nikahisi manukato makali kutoka maungoni mwake huku tabasamu likichanua usoni pake na jino moja sijui la dhahabu au mfano wa dhahabu likajitokeza kinywani mwake.
“Vipi?” hatimaye alisema kwa mnong’ono wa kibiashara zaidi huku akinishika mkono.
Kwa kuwa nilikuwa mwenyeji wa eneo hilo sikuhitaji kujiuliza ni kpi kilichomfanya mwanadada huyu anisimamishe. Watu wa aina yake muda huo huwa wameshatanda kando ya Barabara ya Kinondoni pale Mwembejini, kule kwenye makaburi ya ‘Lang’ata’, kwenye njiapanda ya kuelekea Leaders Club pale Tunisia Road hadi maeneo mengine ya huko Ada Estate wakiwa mawindoni, wakivizia mwanamume ‘mwenye njaa.’
Sikutaka kumjibu vibaya aliyenigeuza mimi kuwa windo lake. “Poa tu,” nami nilimjibu kwa sauti ya chini, nikimruhusu aendelee kukishika kiganja cha mkono wangu na wakati mwingine kukitomasa-tomasa.

“Inakuwaje?” akarusha swali na kumalizia, “twen’zetu basi tuka…” alichomalizia kukitamka kilikaribia kunichekesha kwa kuwa nilitarajia ndivyo angesema.
Hata hivyo sikucheka. Nikaendelea kuonesha kumjali. Nikamjibu kwa upole, “Usijali, tufanye siku nyingine. Leo siko fresh,” nikaongeza huku nikijipapasa mifuko kuonyesha kuwa sikuwa na pesa.
“Una ngapi sh’ngapi?” aliniganda.
“Sina kitu,” kwa kiasi fulani nilianza kuchukia. Hawa viumbe wenye biashara hizi mara nyingi huwa ving’ang’anizi! Na ukiwachekea utajuta!
Akanitazama usoni na kugundua kuwa sasa sikuhitaji kuendelea kujadili kuhusu hiyo hoja yake na wala sikuwa nahitaji kuwa naye. Akaniachia mkono huku kwa unyonge akisema, “Poa, acha sie tukapuyange viwanja…”

Sikumjibu.
Nikaendelea kuvuta hatua taratibu hadi nilipofika kwenye Mtaa wa Ngano. Kama awali mtaa huu ulikuwa umetulia lakini sasa niliona kama ukimya ulizidi. Mara ghafla nikasikia upepo mkali ukivuma, upepo ulioambatana na kimbunga kidogo. Vumbi likatimka mbele yangu, hatua kama kumi hivi. Miti ikatikisika kwa nguvu!
Nikashangaa kisha nikajawa na hofu! Haukuwa upepo wa kawaida!
Mara mbele kidogo, kushoto ambako kulikuwa na kijibaa kidogo chenye wateja wachache kukazuka kelele kali kwa sauti kama ya mwanamke. Punde msichana aliyevaa blauzi pana na suruali akatoka mbio akikimbilia barabarani akija huku nilikokuwa!
Aliponifikia, akanitazama kidogo kisha akanipita na kuendelea kukimbia akielekea Mwembejini. Sikumjali. Nikaendelea kutulia palepale nikiangalia eneo lile la mbele yangu ambako upepo uliokuwa ukivuma sasa ulianza kupungua taratibu.

Hatimaye hali ikatulia, nami nikaanza kutembea tena. Nikavuta hatatua taratibu huku nikihisi kutokuwa na utulivu moyoni.
Nilipofika jirani na kile kijibaa, upepo ukaanza kuvuma tena! Kwa msaada wa mwangaza mdogo wa taa zilizokuwa zikiwaka ndani ya baa hiyo nikafanikiwa kuona kitu kama kamba ndefu mbele yangu. Kamba nyeusi. Nilijenga imani kuwa ni kamba kwa kuwa kitu hicho kilikuwa kimetulia tuli kandokando ya barabara.
Sikuwa na wazo lolote toafuti kuhusu kitu hicho, nikaendelea kutembea hadi nikawa hatua kama mbili hivi kutoka mbele ya kitu hicho.
Haikuwa kamba!

Alikuwa ni nyoka! Na hakuchelewa, alijivuta kwa kasi na kutua kwenye kiganja cha mguu wangu wa kulia, akadonoa haraka kisha kwa kasi ileile akajivuta na kuingia nyasini, kando ya barabara!
Eneo aliloingia kiumbe huyo hatari kulikuwa na ua kubwa lililotengeneza chaka la aina yake hivyo niliishia kusikia sauti ya, “Shhhhh…ssshhhhh….” ishara ya kutokomea ndani ya chaka hilo lililokuwa jirani sana na kijibaa hicho.
Lilikuwa ni tukio la haraka sana na hata maumivu yake pia yalikuja kwa kasi vilevile! Dakika ya kwanza niliweza kukanyaga chini mguu. Nilipovuta hatua moja, nilipokanyaga tena chini maumivu nliyoyasikia hayakuwa ya kawaida! Yalikuwa makali kuliko unavyoweza kukadiria.
Nikahisi uhai unakaribia kunitoka! Jasho likaanza kunitoka! Sikuona mtu yeyote mbele wala nyuma! Maumivu yakazidi! Nikalazimika kuushika mguu ulidungwa jino na joka lile, nikaukunja juu-juu kwa nyuma na kusimamia mguu wa kushoto pekee japo kwa shida.
Nilipozidiwa nikajikuta nikianguka chini, katikati ya barabara huku kwa mbali nikisikia sauti ya mtu akicheka, Sauti ya kike!

NILIANZA kukata tamaa ya kuishi. Simulizi nyingi nilizokwishazisikia tangu utoto kuhusu madhara ya kuumwa na nyoka ziliniletea kumbukumbu ya kuogofya akilini mwangu. Nikatulia chini, katikati ya barabara huku nikiangalia huku na kule na kuomba Mungu atokee mtu wa kunisaidia.
Hatimaye haikutimu hata dakika moja, mtu mmoja, mwanamume akatokea ndani ya kile kijibaa, akitembea kwa kasi lakini akionekana kutokuwa na wasiwasi wowote. Huenda alikuwa akiwahi nyumbani kwake. Aliponiona, akashtuka na kunisogelea.
“Vipi?” ndivyo alivyoniingia.
“Nyoka!” nlimjibu. Sasa maumivu yalikuwa yakizidi na kwa hali hiyo nikawa najikunja na kujikunjua pale chini huku nimeushika mguu uliojeruhiwa.
“Hee!” alibwata kwa mshtuko.”Atakuwa ni yule nyoka tu….duh!”
Akanishika mkono na kunisaidia kunyanyuka. “Jitahidi kujikokota tufike hata pale kwenye ile nyumba.”
Mbele yetu kulikuwa na nyumba ambayo nilisikia kuwa ilikuwa inamilikiwa na Meya wa moja ya manispaa za Jiji la Dar.

Nilitembea kwa mguu mmoja wa kushoto huku wa kulia nimeukunja juu kwa nyuma na jamaa yule kapenyeza mkono wake kwapani kwangu kulia ili kuwa mhimili mzuri wa kutembea.
Nikawa narukaruka hadi kwenye hiyo nyumba ambayo ilikuwa hatua kama kumi na tano au ishirini hivi kutoka pale nilipokumbwa na zahama.
Tulipofika kwenye nyumba ile tukapokewa na binti mmoja na kijana mmoja wa kiume wanaosadikiwa kuwa walikuwa wakiilinda tu nyumba hiyo. Taarifa za kuumwa kwangu nyoka zikazidi kuenea tangu nilipofika hapo. Dakika tano baadaye watu saba walikuwa ndani ya nyumba hiyo, mmoja wao akiwa ni mzungu wa asili ya Uholanzi, ambaye alikuwa akiishi jirani na nyumba hiyo akiwa pia na ofisi ya shirika lake binafsi hapohapo.
Yule mzungu ndiye aliyeonekana kutaharuki zaidi alipoisikia taarifa yangu. Akawa akihaha huku na kule kusaka kamba ya kunifunga mguuni ili sumu isisambae. Vijana wengine waliokuwa pale nao walikuwa wakihangaika kivyao, baadhi yao wakionekana kuogopa kuwa labda nyoka huyo atazuka tena na kumdhuru yeyote kati yao. Baada ya dakika kadhaa mmoja akaja na waya wa umeme na wembe.
“Mchanje kwanza!” mmojawao alisema.
Nikachanjwa juu kidogo ya kiganja cha mguu! Damu nzito kama tope, damu nyeusi tii ikatoka kama mabonge fulani hivi. Wote walioshuhudia wakashtuka! Mimi nikaogopa!
“Chanja tena juu yake!”
Ushauri ukatolewa na mwingine.

Mwenye wembe akachanja mara mbili umbali kama wa inchi tatu, juu ya pale alipochanja awali.
“Heee…” wakazidi kubwata kwa mshangao. Hata hapo ilitoka damu nzito na nyeusi kama tope.
Wakachanja sehemu kama nne tofauti mpaka jirani sana goti na pote pakaonyesha kuwa tayari pameathiriwa na sumu ya joka lile.
Mguu ukatapakaa damu! Haukupendeza kutazamwa! Mabonge bonge hayo ya damu yakawa yakishuka taratibu na kunitisha hata mimi mwenyewe!
Kilichonitia woga ni kuwaona hata hawa vijana waliokuja kunisaidia nao wakionekana kutaharuki. Baadhi walikuwa wakinikodolea macho tu bila ya kufanya chochote.
Hatimaye yule aliyekuwa akinichanja mguuni akasema, “Kunja suruali zaidi bro!”

Nikafanya alivyotaka. Nilikunja suruali hadi mapajani.
Akachanja kwenye paja mara tatu. Damu iliyotoka hapo ni ile ambayo wenyewe tumeizoea kuwa ni damu ya mwanadamu yeyote. Haraka jamaa huyo akaamua kuitumia kamba ya katani iliyokuwa imeletwa hapo na kijana mmoja wa Kiarabu ambaye alitoka kwenye nyumba kama ya tano hivi baada ya kusikia kuhusu tukio hilo.
Nikafungwa kamba hiyo kama vile ni mtu ninayezuiwa kutoroka. Ilikazwa kisawasawa kwenye paja ikiaminika kuwa itasaidia kuizuia sumu kupanda zaidi na kuleta madhara zaidi.
Kilichofuata ni kukabidhiwa fimbo ya kunisaidia kutembea mpaka nje, kando ya barabara ambako yule kijana wa Kiarabu alikuwa kaegesha gari dogo aina ya Toyota Mark 11 na nikaingia ili wanipeleke hospitali.
“Usihofu tena,” yule kijana wa Kiarabu ambaye nilikuwa nimeketi naye katika kiti cha nyuma aliniambia. Kisha akavuta suruali juu na kunionyesha mguu wake wa kushoto ulivyobabuka! Ulikuwa unatoka magamba kuanzia chini mpaka kwenye goti!
“Unaona hii?!” aliniuliza huku akinitazama usoni kwa macho makali.
Sikumjibu, nikautazama tu ule mguu, tendo nililoamini kuwa lilitosha kumfanya ajue kuwa nimemsikia.

itaendeleaaaa

No comments