| Simulizi | ZAWADI YA MAMA.

Share:

     Mama mmoja alipoona siku zake za kuishi duniani zimekaribia alimwita mwanae wa pekee wa kiume na akisha kuchukua mafiga matatu Pamoja na vijiti vitatu alifungua kinywa chake akamwambia:

"Mwanangu nimekuita hapa ili nikueleze mambo ya busara yatakayo kusaidia katika maisha yako ya baadaye. Mama yako umri umenitupa mkono na hivyo sina budu kukupandikizia kitu kabla sijaondoka na kukuacha peke yako duniani. Nimeamua kufanya hivyo hii ni kwa sababu nataka usije ukalaumiwa na watu kwamba hukufundwa na mama yako na ndio maana uko hivyo ,sasa mwanangu kabla sijaanza kukuusia haya maneno nakuomba uuweke mkono wako  wa kulia kifuani mwangu.

Mwanangu najua sasa hivi umeshafanikiwa kupata kazi serikalini baada ya kuhitimu masomo yako ya chuo kikuu.Si kwamba ulikuwa na akili sana hadi ukafanikiwa kuipata hiyo elimu na hiyo kazi hapana ila ni kwa neema ya Mungu tu,Maana kuna vijana wengi sana ulioanza nao Lakini kwa changamoto za hapa na pale hawakuweza kuimaliza safari salama bali walikata tamaa na hivyo kuwafanya waishie njiani. Wewe Mungu kakusaidia kuimaliza safari yako salama na hatimaye Leo umepata kazi nakusihi sana usimuache Mungu Katika Maisha yako ,mfanye kuwa kipaumbele chako cha kwanza yaani mtangulize mbele Katika kila jambo unalotaka kulifanya ili akupiganie zaidi na zaidi. Mwanangu umepata kazi hii ambalo ndilo jambo la kufurahisha na la bahati sana,sasa nakuomba anza kwa kujijenga kiakili na kiuchumi ili Maisha yako yawe mazuri, usikimbilie kuoa kabla hujayafanya hayo bali yatimize kwanza ndipo umlete mwanamke wako ndani ya nyumba .Nunua kiwanja chako jenga nyumba yako ili uishi Maisha ya furaha pasipo usumbufu wa aina yoyote ile,,na usiutegemee sana mshahara wako kwa kila kitu kilichopo mbele yako au kinachokukabili,anzisha miradi yako tofauti tofauti na ikiwezekana unanunua na mashamba ya kutosha ili yawe yanakusaidia hususani kwenye kulitatua tatizo la chakula na hivyo kuuacha mshahara wako ukijidhatiti kwenye mambo mengine mhimu .

Mwanangu usiwe mtu wa dharau na ubinafsi dhidi ya jamii inayokuzunguka.Ishi na watu kwa upendo na amani na shirikiana nao kwa kila hali,katika shida na raha.Waheshimu Maskini  na  matajili na ukitupilie mbali kitu kinachoitwa ubaguzi ili amani katika maisha yako ya kila siku izidi kunawiri na kububujika kila uchao.Mwanangu tafuta marafiki wanaokufaa na wenye nia njema ya kimaendeleo, usiwe na marafiki wenye wivu na wanaopenda unafiki na kutokupenda kumwona mwenzao akipiga hatua kimaisha, hao waepuke na uwaogope kama ukoma. Harafu cha msingi Mwanangu ninachotaka kukuambia, ni kwamba uangalie sana mshahara wako wa kwanza kwa umakini sana na kwa macho angavu Maana huo ndio utakaokufungulia njia ya wewe kuitwa mbarikiwa.Usije ukadhubutu hata siku moja kuupeleka kwa mganga wa kienyeji, uchukue wote piga hatua ukamtolee Mungu wako na hapo ndipo utakapo ziona Baraka zikimiminika maishani mwako na hakuna kitakacho kuharibikia.

Kingine ninachotaka kukuambia ni hiki .Muda wa wewe kuoa ukiwadia omba sana Mungu akupatie mke mwema mwenye nia njema na wewe na mwenye tabia njema.Usiangalie sura,umbo au rangi ya mwili,angalia tabia Maana uzuri wa mwanamke ni tabia na si umbo au sura. Ukifanikiwa kumpata mwanamke wa ndoto zako tafadhari sana mpende na umtii na wala usimnyanyase na kumfanya kuwa MTU wa majonzi na kilio kila  kunapoitwa leo ,,usipende kumpiga piga kama ngoma bali wewe mpende na umheshimu kama mama watoto wako ili na yeye ajione wa thamani sana chini ya jua .Kumbuka tu wanawake wengi hupenda kufurahishwa na kupendwa na wanaume wa ndoto zao .Shirikiana nae katika mambo ya kuinua maendeleo ya kifamilia.Fanyeni kazi kwa ushirikiano kama haya mafiga yanavyofanya kazi kwa pamoja ,pia muwe na umoja kama hivi vijiti Maana Siku zote kidole kimoja hakiwezi kuvunja chawa.Simamia msimamo wako wenye  malengo chanya na usikubali kuendeshwa na mtu ,ila sikiliza ushauri wenye nia njema na usiusikilize ushauri wenye nia mbaya ya kubomoa.

Cha mwisho ilinde sana ndoa yako na usikubali ivunjwe na watu wasiopenda maendeleo ya ndoa za wenzao,na katika kulitekeleza hili usiyasikilize maneno ya watu bali wewe msikilize Mungu tu maana yeye ndiye atakaye ilinda na kuisimamia ndoa yako.Ukifanikiwa kupata watoto walee na uwaongoze Katika kuyashika maadili yaliyo mema .Watunze na hakikisha unawapatia elimu ya kiroho na kidunia ili uwasaidie katika kuzikamilisha ndoto zao na malengo yao kwa Maisha yao ya baadaye. Mwanangu mwendo nimeumaliza,vita nimevipigana na imani nimeilinda na usukani wa kuyaendeleza Maisha ya hapa duniani nimekuachia,,Dereva mwema ni yule anayewafikisha abiria wake salama, kwa hiyo yazingatie sana hayo niliyokueleza.Ukiyachukua na kuyaweka moyoni kamwe hutokaa na kujuta katika maisha yako yote ya hapa duniani .Mimi nimemaliza na mikono yangu nimenawa,sasa unaweza kuutoa mkono wako juu ya kifua changu ".

Baada ya kuyaongea hayo yule mama alikata roho,na hivyo akatangulia ahera Akiwa mweupe, kiroho safi maana yote aliyopaswa kuyatimiza kabla ya kifo chake aliyatimiza yote mbele ya mwanae. Kijana alifanikiwa kumsindikiza mamae kwa amani hadi kaburini huku akiapa kuyafuata yote aliyoachiwa na mama yake ENZI za uhai wake.

Hivi sasa Kijana anaishi kwa amani na maisha yake yametawaliwa na furaha Yaani furaha kwake, watoto wake pamoja na mkewe Maana aliyazingatia mausia ya mama yake.

     ===>Sasa Kama na wewe umeguswa na wosia huu acha neno hapo chini la " MAMA NI MAMA" ili kuwaombea wanawake wote wenye mioyo kama hii ya busara, Mungu awabariki na awape amani tele huko waliko hata kama watakuwa wameshatangulia mbele ya haki.

No comments